Saturday, 31 March 2018

Mwisho wa mateso


The End of Torture (Mwisho wa Mateso) - 42

MATATIZO bado yanaendelea kuyaandama maisha ya msichana mdogo, Amelia. Dhiki, mikosi na mabalaa vinaonekana kuwa sehemu ya kawaida ya maisha yake kiasi cha kumfanya atamani kufa. Anafanya jaribio la kutaka kufa kwenye kimbunga hatari cha Agripina lakini inashindikana.
Amelia alifanyiwa vipimo mbalimbali na baada ya Daktari Mwashiga kuridhishwa na afya yake, alitoa damu. Baada ya zoezi hilo kukamilika, damu hiyo ilichukuliwa mpaka wodini ambapo daktari alianza kuiandaa kwa ajili ya kumuongezea mtoto wa Amelia.
Katika hali ambayo hakuitegemea, Daktari Mwashiga aligundua kitu kilichomshangaza sana kuhusu damu hiyo. Kulikuwa na tofauti kubwa ya vitu ambavyo kitaalamu huitwa ‘antigens’ kwenye damu ya Amelia ukilinganisha na mwanaye, jambo ambalo siyo la kawaida. Hata makundi ya damu zao yalikuwa tofauti lakini hilo halikumshangaza sana kwani inatokea mara nyingi mama akawa na kundi la damu ambalo ni tofauti na la mtoto anayemzaa. Kilichomshangaza ni utofauti wa antigens.
Daktari Mwashiga alirudia tena kuichunguza damu hiyo lakini majibu yalikuwa yaleyale. Ikabidi atoke na kwenda kumuita Amelia ambaye alikuwa wodini, akiwa amelala pambeni ya mwanaye.
“Nakuomba ofisini kwangu mara moja,” alisema daktari huyo na kumshika mkono Amelia, akaenda naye mpaka ofisini kwake na kumkaribisha kiti, akakaa na kuanza kumuuliza maswali mbalimbali, lengo likiwa ni kutaka kujua historia yake kwa ufupi na jinsi alivyompata mtoto huyo.
Hakuna jambo ambalo lilikuwa likimuumiza Amelia kama kuanza kueleza historia ya maisha yake. Kila alipokuwa akikumbuka mambo yaliyomtokea maishani, alikuwa akiumia sana ndani ya moyo wake.
Hata hivyo, kwa kuwa ilikuwa ni lazima aeleze ili daktari ajue nini cha kufanya, Amelia hakuwa na namna zaidi ya kumueleza ukweli. Akamsimulia historia ya wazazi wake kwa ufupi na jinsi walivyokufa na kuwaacha yeye na mdogo wake wakiwa yatima.
Hakuishia hapo, alieleza pia jinsi mdogo wake huyo alivyokufa kwa kukosa matibabu baada ya kushambuliwa na malaria kali. Alipofika hapo, alishindwa kuendelea kutokana na uchungu aliokuwa anauhisi, akawa analia kwa kwikwi.
Baada ya kubembelezwa sana na Dokta Mwashiga ambaye alikuwa akimpa maneno ya kutia nguvu na ushauri nasaha, Amelia alitulia na kuendelea kueleza jinsi alivyokutana na mwanaume mtu mzima, Mafuru ambaye ndiye aliyemjaza ujauzito baada ya kumrubuni kwa kipindi kirefu.
“Siku niliyomwambia kuwa nina mimba ndiyo ukawa mwisho wa kumuona, nimeteseka sana mwenyewe, faraja pekee ikiwa ni mdogo wangu kabla hajafa,” alisema Amelia na kufuta machozi, akashusha pumzi ndefu na kuendelea kueleza kuwa shida na matatizo aliyopitia yalimfanya atamani kufa.
“Serikali ilipotangaza kwamba kimbunga Agripina kinakuja, ujauzito wangu ulikuwa na miezi tisa, nikaona bora nife kwenye kimbunga na mwanangu kwa hiyo sikuondoka kama serikali ilivyotangaza,” alisema Amelia, jambo ambalo lilimshangaza sana Dokta Mwashiga.
Akakaa vizuri kwenye kiti chake na kuendelea kumsikiliza ambapo alieleza jinsi kimbunga hicho kilivyopiga na kumkuta akiwa kwenye harakati za kujifungua. Aliendelea kueleza kila kitu kilichotokea mpaka alipojikuta akiwa kwenye Hospitali ya Jeshi ya Lugalo.
Akaeleza jinsi alivyohangaika kumtafuta mwanaye hadi alipokuja kupatikana akiwa hai. Mpaka hapo tayari Dokta Mwashiga alishaanza kupata picha kwamba inawezekana kabisa mtoto ambaye msichana huyo alipewa hakuwa wake. Hata hivyo hakumkatisha, alimuacha aendelee kusimulia kila kitu mpaka alipomaliza.
Alipomaliza, na yeye alimwambia sababu iliyomfanya amuulize kuhusu historia yake ambapo alimueleza kwamba amebaini kuna tofauti kubwa ya antigens na makundi ya damu kati yake na mwanaye. Akamueleza kuwa damu aliyojitolea, haiwezi kumfaa mwanaye kwa sababu walikuwa hawaendani, kauli ambayo ilimshangaza sana Amelia.
Ilibidi daktari huyo aanze kumueleza kwa kina jinsi damu ya mama na mwanaye inavyotakiwa kuwa. Alitumia lugha nyepesi kumfafanulia mambo mbalimbali kuanzia jinsi baba na mama wanavyochangia damu ambayo baadaye ndiyo inakuja kuwa ya mtoto atakayezaliwa.
Hata hivyo, Amelia hakutaka kuelewa chochote, akawa anang’ang’ania kuwa huyo mtoto ni wake na huenda Mungu amempa maradhi hayo kwa makusudi ili kumpitisha kwenye majaribu. Akajiapiza kuwa atampenda na kuyapigania maisha yake kwa kadiri ya uwezo wake wote.
Kwa kuwa suala la msingi lilikuwa ni kupata damu ya kumuongezea mtoto huyo, Daktari Mwashiga alimruhusu Amelia arudi wodini kwa mwanaye wakati yeye akiendelea kutafuta njia nyingine za kumsaidia. Kwa bahati nzuri, ilipatikana damu ambayo ilikuwa ikiendana naye.
Akatundikiwa chupa ya damu ambayo ilianza kutiririka kwa kasi kuingia kwenye mishipa yake. Licha ya kuonesha msimamo wake mbele ya daktari huyo, Amelia aliendelea kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu. Haikumuingia kabisa akilini mwake kuambiwa kwamba mtoto huyo hakuwa wa kwake.
Kwa jinsi alivyokuwa anampenda licha ya matatizo aliyokuwa nayo, aliendelea kujiapiza kuwa hata iweje, hawezi kukubali kutenganishwa naye. Chupa ya damu iliendelea kutiririka kuingia ndani ya mwili wa mtoto huyo na baada ya kuisha, aliongezewa ya pili.
Baada ya kuongezewa damu ya kutosha, hali yake iliendelea kuwa nzuri, akaanza kuchangamka, jambo ambalo lilimfurahisha sana Amelia. Siku zikawa zinazidi kusonga mbele huku afya ya mtoto huyo ikizidi kuimarika. Ile furaha ambayo ilitoweka kwa kipindi kirefu kwenye maisha ya msichana huyo mdogo ikaanza kurejea taratibu.

***
Nisingependa kumaliza hadithi hii ya leo bila kukumbusha jambo muhimu la kutoa maisha yako kwa Mungu. Maisha tuliyonayo hapa duniani ni mafupi sana, yanapita kama maua yachanuavyo na kunyauka. Wengi unaowafahamu wamekufa lakini wewe unapumua, ni vyema basi kufikiria maisha baada ya kifo.
Kila siku jiulize: “Hivi nikifa leo nitakwenda jehanam au peponi?” Kila mmoja wetu analo  jibu lake, bila shaka sote tungependa kwenda peponi. Kama hivyo ndivyo, basi tiketi ya kwenda huko ni matendo mema na kujiepusha na uovu.
Tukumbuke mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele.

Je, nini kitafuatia? Usikose Alhamisi ijayo kwenye Gazeti la Amani.

No comments:

Post a Comment